WELCOME YOU ALL TO MY NEW BLOGS

Visiting this blog will help you to learn more about the laws of Tanzania and its related matters.

Friday, June 22, 2012

Mwenendo Kesi ya Lulu


Mawakili wa Serikali wamkaanga Lulu Send to a friend
Thursday, 21 June 2012 19:52
James Magai
MAWAKILI wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kuthibitisha kwamba umri wa msanii wa filamu Elizabert Michael ni zaidi ya miaka 18.Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na mawakili wawili; mmoja wa Lulu na mwingine wa Serikali ambao hawakutaka kutajwa, zimeeleza kuwa vielelezo hivyo vimewasilishwa jana mahakamani hapo.

Habari zimeeleza kuwa moja ya vielelezo hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja nchini.
"Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, alisema mmoja wa mawakili hao.

 Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana.

 Baada ya vielelezo kesi hiyo itasikilizwa Juni 25 mwaka huu. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.

Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.

Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili kulinda maslahi yake.

 Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali yenyewe kufanya uchunguzi huo kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao.

 Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.

 Lakini taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.

Viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17.

Viapo hivyo ambavyo Gazeti hili limefanikiwa kuviona ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa  Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.

Viapo  vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995  katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.
Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa,  mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.

Viapo hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama, baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael Kimemeta .

“ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika Kanisa la Katoliki  Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa.

Utata wa umri wa mshtakiwa huyo uliibuka Mei 7, 2012 katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya wakili wake Fungamtama kudai kuwa ana miaka 17 na hivyo kuomba kesi yake isikilizwe katika mahakama ya watoto.

Hata hivyo Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina mamlaka ya kuyashughulikia na kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahamaka Kuu.

Ndipo Mei 15 wakili Kibatala aliwasilisha maombi hayo mahakama kuu wakiomba mahakama hiyo iamuru kwamba Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kisheria kushughulikia maombi hayo.
Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka 2012,  pia mawakili hao waliomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kufanya wala kuagiza uchunguzi huo ufanyike, basi Mahakama Kuu yenyewe ama iagize au ifanye uchunguzi huo.

Sambamba na hayo pia waliomba Mahakama Kuu iamuru mwenendo wa kesi ya msingi katika Mahakama ya Kisutu usimamishwe hadi suala la umri litakapopatiwa ufumbuzi.

Katika uamuzi wake Jaji Dk. Fauz Twaib alisema kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kushughulikia maombi hayo na kwamba ilikosea kukataa kuyashughulikia.

Pia Jaji Dk. Twaib  alikubaliana na hoja za pingamizi la awali la wajibu Maombi(Jamhuri) kupitia kwa Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro akisaidiana na Wakili Elizabeth Kaganda, walizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Mei 28,2012.

 Wakili Kimaro alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo kinyume cha sheria na kwamba hata vifungu vilivyotumika katika madai hayo haviipi Mahakama Kuu uwezo wa kuyashughulikia.
 Hata hivyo licha ya kukubali kuwa maombi hayo yaliwasilishwa mahamakani isivyo sahihi, lakini Jaji Dk. Twaib alisema bado Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuyashughulikia.

 Chini ya kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Dk. Twaib aliuagiza upande wa mwombaji(mawakili wanaomtetea mshtakiwa), kuwasilisha mahakamani hati hizo za viapo na vielelezo vya umri wa mshtakiwa huyo juzi.
Source: Mwananchi Communication

Ensuring Fair Trial in Cases of Children in Conflict With the Laws: The Tanzanian Paradox







PREFACE
The Issue of managing or dealing with children coming into conflict with the law has historically haunted nations and Tanzania is no exception. Although there have already been important headways, much remains to be done in ensuring a child friendly justice system in Tanzania.
The problem has for ages risen when children come in contact with a justice system that is unresponsive to their needs, which not only deprives them of their liberty, but also accentuates or increases their vulnerability to abuse, violence, exploitation and health related risks such as injury and HIV infection.
This work comes in place to analyze the legal and institutional framework under the International, regional and national (Tanzanian) levels; with a view of determining as to how much consistent are they with the accepted legal standards. It however ends by recommending a Child friendly justice system which aims at restorative justice.


To read the full article go to this link
http://works.bepress.com/lucky_mgimba/7/



Wednesday, June 20, 2012

Majaji Wapya Kumi Waapishwa Yumo Wakili wa Lulu


Tuesday, 19 June 2012 21:30
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, akimuwaapisha Mhe. Semistocles Simon Kaijage wa Mahakama Kuu kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani. Sherehe hizo zimefanyika Ikulu
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, akimuwaapisha Mhe. kipenka M. Musa, jaji wa Mahakama Kuu kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani. Sherehe hizo zimefanyika Ikulu



Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  akimuwaapisha Mhe. Edward Mukandara Kakwezi Rutakangwa, Jaji wa Mahakama ya Rufaa kuwa miongoni mwa makamishna wa tume ya Mahakama.Sherehe hizo zimefanyika Ikulu

Leon Bahati 
RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea, Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu)  anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
De-Mello ni miongoni mwa mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu.

Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

Akizungumza kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Majaji wengine walioapishwa jana na Rais Kikwete ni Francis Mutungi, John Mgeta, Patricia Fikirini, Sam Rumanyika, Salvatory Bongole, Jerald Alex, Mathew Mwaim, Jacob Mwambegele na Latifa Mansook.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema amefurahi kuteuliwa kwa majaji hao na anawafahamu kuwa wote ni wazoefu na watatekeleza kazi zao kikamilifu.

“Wote ni wazoefu. Ukiangalia utaona kuwa sita walikuwa wakifanya kazi mahakamani (Mahakama Kuu na Rufani), wawili mawakili wa kujitegemea na wawili pia mawakili wa Serikali,” alisema Jaji Othman.
Alisema majaji hao wote kabla ya kupangiwa kazi rasmi itabidi waanze kufanya kazi ya kukabiliana na kesi zaidi ya 2,200 zilizopo katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi.

Uteuzi wa majaji hao 10, alisema unaifanya Mahakama Kuu sasa kuwa nao 69 tofauti na wale 16 wanaounda Mahakama ya Rufani.
Othman alisema pamoja na uteuzi huo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kulundikana kwa kesi nyingi kuliko uwezo wao.
“Walioteuliwa watasaidia lakini ukweli ni kwamba bado tunakabiliwa na upungufu wa majaji. Kesi ni nyingi,” alisema Othman.

Hakuweza kueleza mara moja idadi kamili ya majaji inayotakiwa ili kukidhi mahitaji lakini akasema kuwa Serikali imeliona hilo na imekuwa ikilifanyia kazi hatua kwa hatua.

Licha ya upungufu wa majaji, Jaji Othman alisema wanakabiliwa na tatizo la kutumia teknolojia ya zamani ya kusikiliza na kuandika tofauti na maendeleo ya sasa ambayo yanahitaji kurekodi.
“Mfumo huu wa kutumia teknolojia ya kisasa pia ungeweza kuharakisha kesi,” alisema Jaji Othman lakini akasema Kitengo cha Biashara tayari kimeanza kuifanyia kazi teknolojia ya kisasa.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, alisema mtu anaweza kutumia simu yake ya mkononi kujua siku ya kesi yake na hata kuperuzi kwenye mtandao kupata hukumu pamoja na mwenendo wa kesi yake. 
Alisema wanatarajia kwenda hatua kwa hatua ili kuhakikisha teknolojia hiyo ya kurahisisha kazi za mahakama inaenea idara zote za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Majaji wengine wapya nao walisema kwenye mahojiano na waandishi wa habari kwamba moja ya changamoto ni kufanya kazi katika mazingira magumu na wingi wa kesi zilizolundikana katika mahakama hiyo.
Jaji Mutungi alisema yeye anaamini kiu kubwa ya Watanzania ni kupatiwa haki na kwamba haki hiyo inapocheleweshwa pia ni tatizo jingine.

Ili kuhakikisha anawatekelezea Watanzania haki zao, Mutungi alisema atajitahidi kufanya kazi kwa bidii na kumaliza kesi nyingi kwa haraka.

Kwa upande wake, Jaji Mgeta alisema pamoja na wingi wa kesi kazi kubwa wanayopaswa kuifanya ni kuwa waadilifu na watenda haki.

Alikiri kwamba Tanzania wako nyuma katika teknolojia ya kuendesha kesi lakini akasema hilo halipaswi kuwa ni jambo ambalo litawafanya warudi nyuma na kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.
Source (Habari): Mwananchi Communication
Source (Picha): website ya mahakama  (http://www.judiciary.go.tz/) 

Thursday, June 7, 2012

MHE. JAJI EUSEBIA NICHOLAS MUNUO Amechaguliwa Kuwa Mwenyekiti "International Association For Women Judges" Duniani


MHE. JAJI EUSEBIA NICHOLAS MUNUO Amechaguliwa Kuwa Mwenyekiti "International Association For Women Judges" Duniani

 

MHE. JAJI EUSEBIA NICHOLAS MUNUO amechaguliwa kuwa Mwenyekiti "International Association for Women Judges" duniani. Mkutano huo umeanza tarehe 27/4 - 9/5/2012. Wadhifa huo ni heshma kwa Tanzania na Mahakama ya Tanzania
Source: http://www.judiciary.go.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=138%3Amhe-jaji-eusebia-nicholas-munuo-amechaguliwa-kuwa-mwenyekiti-qinternational-association-for-women-judgesq-duniani&Itemid=1

Tuesday, June 5, 2012

Upelelezi kesi ya Lulu bado haujakamilika


Monday, 04 June 2012 21:19
Tausi Ally na James Magai
UPELELEZI wa kesi ya mauaji inayomkabili muigizaji nyota wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu bado haujakamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 

Lakini jana Wakili wa Serikali, Peter Sekwao aliieleza mahakaama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo na hadi Juni 18, 2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alilazimika kupandishwa kizimbani mara mbili baada ya tarehe ya kutajwa tena kukosewa.

Awali, hakimu Mmbando alisema kuwa kesi hiyo ingetajwa tena Juni 28 kisha mshtakiwa huyo akaondolewa mahakamani na kupelekwa mahabusu akisubiri kurejeshwa mahabusu ya gereza la Segerea.
Lakini baadaye alirudishwa tena mahakamani na kupandishwa kizimbani baada ya kubainika kuwa tarehe iliyopangwa ya kutajwa kwa kesi hiyo haikuwa sahihi kwani karani alikuwa amekosea kuhesababu, ndipo ikapangwa Juni 18.

Jalada hilo lilipelekwa Mahakama Kuu Ijumaa ya Mei 18, mwaka huu baada ya jopo la Mawakili wa mshtakiwa  huyo kuwasilisha maombi juu ya uchunguzi kuhusiana na umri halali wa msanii huyo.

Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata kama ni mtoto au ni mtu mzima, jambo ambalo limewalazimu mawakili hao kuwasilisha maombi hayo ya uchunguzi wa umri wake Mahakama Kuu.Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili Peter Kibatala Mei 15, 2012 na yamepangwa kusikilizwa  na Jaji Dk Fauz Twaib Mei 28, 2012.

Mawakili wa mshtakiwa huyo walifikia uamuzi wa kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu baada ya kugonga mwamba Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabla ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu, mawakili hao waliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 7,2012  wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa bado ni mtoto.

Mawakili hao walidai mahakamani hapo kuwa msanii huyo ana umri wa miaka 17 na kwamba kwa maana hiyo yeye bado ni mtoto na kesi yake haipaswi kusikilizwa katika mahakama za kawaida kama mtu mzima. 
Kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea msanii huyo, wakili Kenedy Fungamtama alidai kuwa mteja wao ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyotamkwa mahakamani.

Alidai kuwa hata cheti cha kuzaliwa walichokiwasilisha mahakamani kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa hivyo kuwa na umri wa miaka 17.

“Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatafsiri kuwa mtoto ni yule aliyekuwa na umri chini ya miaka 18 hivyo katika suala la mteja wetu alipaswa kushtakiwa katika mahakama ya watoto,” alidai Wakili Fungamtama.

Hata hivyo upande wa mashitaka kupitia kwa wakili Elizabeth Kaganda ulipinga maombi hayo na kudai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na hivyo kuomba wapewe muda zaidi.
Wakili Kaganda pia alidai kuwa hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa huyo linasomeka kama Diana Elizabeth wakati mshtakiwa huyo ametajwa mahakamani hapo kama Elizabeth Michael.

Akijibu hoja hiyo, wakili Fungamtama alikiri jina hilo kusomeka Diana Elizabeth na kusema kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa wakristo kuwa na majina mawili.
Katika uamuzi wake, Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo alisema kesi hiyo bado iko kwenye upelelezi na kwamba kulingana na jinsi ilivyo isingekuwa busara kuamua hoja yoyote.
Hivyo Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo, aliutaka upande wa utetezi uwasilishe maombi hayo kupitia Mahakama Kuu.

Katika maombi  namba 46 ya mwaka 2012, mawakili hao wanaomtetea msanii huyo wanaiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo.

Jopo la mawakili hao maarufu linadai kuwa linaamini kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo kwa sasa ndio bado inayoshughulikia kesi hiyo, ina mamlaka ya kufanya au kuamuru ufanyike uchunguzi wa umri mshtakiwa huyo. 

Lakini pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Akifafanua juu ya maombi hayo Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) alisema kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa.

Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  ili mahakama iweze kujiridhisha kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kujipa angalizo juu ya maslahi ya mtoto.

“Baada ya uchunguzi huo mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria hiyo ya mtoto,” alisema Wakili Kibatala.

Kwa mujibu wa Wakili Kibatala kifungu hicho ambacho huelezea ulinzi wa maslahi ya mtoto katika uendeshaji wa kesi kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Mbali na Kibatala na Fungamtama ambaye pia anaitetea Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans dhidi ya Tanesco, mawakili wengine katika jopo hilo ni Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo.

De-Melo ambaye amewahi kuwa Rais TLS, pia ni mshindi wa  wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King. 

Jopo la mawakili hao wanaomtetea msanii huyo linahitimishwa na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Source: Mwananchi comunication